Daima Tutamkumbuka Mwalimu Rehema: Mmoja wa vinara Mahiri wa Hedhi Salama Nchini Tanzania

News
Rehema 1

Mwanzilishi wa kampuni ya Kasole Secrets, Hyasintha Ntuyeko & WSSCC National Coordinator Wilhelmina Malima

Mwaka 2013, Mwalimu Rehema Darueshi alihamishwa na kuanza kufundisha shule ya msingi Toa Ngoma iliyopo wilaya ya Kigamboni, mkoani Dar-es-Salaam nchini Tanzania. Mwl Rehema hakuridhika sana na mazingira ya kazi kwani shule hiyo haikua kabisa na watoto wasioona na yeye alikua ndie mwalimu pekee asieona shuleni hapo. Mwalimu Rehema aliamua kuanza kutafuta watoto wasioona kwa kutembelea nyumba zenye watoto wenye ulemavu akiwaomba wazazi wawaruhusu watoto wao kujiunga na shule ya msingi Toa Ngoma ambapo yeye binafsi alijitolea kukaa na watoto hao nyumbani kwake ili wawe karibu na shule.

Mwalimu Rehema alifanikiwa kuongeza idadi ya wanafunzi wasioona shuleni Toa Ngoma kutoka mwanafunzi mmoja hadi kufikia wanafunzi 35. Na huu ndo ulikua mwanzo wa kazi nyingi za mfano zilizofanywa na shujaa huyu katika kuwajengea uwezo watu wenye ulemavu.

Kutokana na ongezeko la wanafunzi shuleni hapo, Mwalimu Rehema aliishawishi wizara ya elimu kuwaongezea walimu 3 na hivyo kuanzisha idara ya elimu maaalumu shuleni hapo; hakuishia hapo; aliendelea kuisihi wizara ya elimu- kitengo cha elimu maalumu kuwajengea mabweni, bwalo la chakula na kuongeza madarasa matatu kwa ajili ya watoto wasioona ili wakae karibu na shule na kwa nafasi kwani hakuweza tena kuendelea kuishi na hawa wanafunzi wote katika nyumba yake ndogo.

Mwalimu Rehema, aliona tatizo la Hedhi Salama kwa watoto wenye ulemavu ni kubwa sana na ukizingatia watoto hao wengi wanatoka katika familia duni sana.

Hivyo aliamua kutafuta msaada kwa wadau mbalimbali kwa kushirikiana na Hyasintha Ntuyeko, mwanzilishi wa kampuni ya Kasole Secrets ambae alifadhili mafunzo ya Hedhi Salama kwa walimu nane na vijana watano wasioona. Baada ya mafunzo hayo, Mwalimu Rehema pamoja na walimu wenzake na vijana wakufunzi walijitolea muda wao kufundisha wanafunzi katika shule mbalimbali za walemavu nchini changamoto ya kutokuwepo kabisa kwa vitabu vya kujisomea kuhusu Balehe na Hedhi Salama kwa maandishi ya nukta nundu kwa watoto wasioona, kulimfanya mwalimu huyu na timu yake wakae chini na kuanza kuchapa vitabu hivyo, kazi iliyopokea ufadhili kutoka WSSCC, UNICEF, SAWA, Plan International & Grow and Know.

Rehema alikua ni mwezeshaji wa kitaifa wa Elimu ya Hedhi Salama: pia alishiriki kama muwezeshaji katika mkutano wa SADC uliofanyika Tanzania mwishoni mwa mwaka 2019. Fursa hii ilimpatia nafasi ya kuwasilisha kazi zake na pia kukutana na wawezeshaji wengine kutoka nchi mbalimbali. Uchapishaji wa vitabu vya Balehe na Hedhi Salama katika maandishi ya nukta nundu ilikua ni moja ya kazi zake bora zilizopengezwa sana na washiriki wa SADC

Mwaka 2018, Mwalimu Rehema alipata tuzo ya I CAN AWARD kutoka Dr.Reginald Mengi Foundation tuzo hii ilitokana na mchango wake mahiri katika kuhudumia jamii ya watu wenye ulemavu. Rehema alikua na ndoto ya kuanzisha  kikundi kazi kwa ajili ya walemavu wa aina mbalimbali ili washughulikie kwa kina suala la hedhi salama na hivyo kuweza kuwafikia walemavu wengi zaidi nchini.

Maisha ya Mwalimu Rehema yaliwagusa wengi hasa wale aliofanya nao kazi kwa karibu. Wilhelmina Malima , WSSCC National Coordinatior, anakumbuka jinsi Rehema alivyokua mstari wa mbele katika kupigania afya na haki za walemavu hasa  katika janga zima la COVID-19:

 Rehema amefanya mengi na alikuwa na ndoto nyingi katika kuboresha maisha ya watu wenye ulemavu hasa wasioona. Alifanya kazi kwa uweledi mkubwa na wiki chache kabla ya kifo chake alikua akitayarisha awamu ya pili ya vipeperushi vyenye maandishi ya nukta nundu kwa ajili ya kuelimisha wasioona jinsi ya kujikinga na COVID-19, awamu ya kwanza ya vipeperushi hivi alishavigawa.  Rehema alisema “Ni vyema tukaendelea kuwasisitiza wale wanaotusaidia kuendelea kua makini ili wasituhatarishe au kutuambukiza COVID-19. Watu wenye ulemavu kama wangu mara zote tunahitaji watu wa kutushika mkono”

Hyasintha Ntuyeko atamkumbuka Rehema kwa umahiri na uthubutu wake; alihakikisha kazi zake zinaongeza thamani katika maisha ya watu wenye ulemavu kila siku:

 Hakika mwalimu huyu alikua ni mfano wa kuigwa katika jamii; Mchango wake katika kuhakikisha kuna kuwepo na usawa wa Elimu, huduma na mazingira rafiki kwa wanafunzi wenye ulemavu hauna kipimo; na hakika mchango wake utaendelea kunufaisha vizazi hadi vizazi.  Hakujua kulalamika wala kukata tamaa hata pale kazi ilipokua ngumu, siku zote alipambana kutafuta suluhu na kwa kweli Mwalimu Rehema alitumia muda wake mwingi kuhamasisha wadau na kutafuta suluhu za changamoto kwa watu wenye ulemavu ili kuhakikisha hawaachwi nyuma.